Madhumuni ya Kozi

Madhumuni ya kozi hii ni kuwapatia wanafunzi mbinu za ubunifu wa kazi za kifasihi na stadi za msingi za uandishi wa kazi za kubuni katika Kiswahili. Kozi hii pia inalenga kuwajengea wanafunzi ari ya kupenda kazi za uandishi wa kubuni katika nyanja zake mbalimbali.

 

Maelezo ya Kozi

Kozi hii inashughulikia kumbo nne za uandishi wa kubuni: hadithi fupi, riwaya, tamthilia na ushairi. Inawajuvya wanafunzi sifa muhimu, mawanda na matatizo ya uandishi wa kazi za kubuni za kumbo hizi. Vilevile, kozi inazingatia mchakato wa ubunifu pamoja na mahusiano ya kipembuzi baina ya kazi ya ubunifu na halisi; na kati ya mwandishi/msanii na msomaji au mtazamaji na hadhira. Vipengele vya msingi vya nathari, drama/tamthilia na ushairi vinajadiliwa na kutolewa vielelezo kutoka katika kazi za ubunifu za Kiswahili na Kiafrika.